Muda mwingine unaweza kujiuliza kuhusu mafanikio ya mtu ukadhani labda ni juhudi, kipaji au anachapa kazi sana la hasha wakati mwingine tunapaswa kungalia kwa jicho la tatu hasa uhusiano wa huyo  mtu na Mungu.




Jumapili ya Januari 16, Mchungaji wa KKKT, Usharika wa Ubungo Oscar Mlyuka alimwita mbele ya usharika mzima mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Simon Msuva,  ambapo amesema kuwa amezidi kuinuliwa na kuendelea kupata mafanikio kwa sababu hajamuacha Mungu licha ya umaarufu wake pamoja na mafanikio makubwa aliyokwisha kuyapata.


 “Msuva akiwepo nchini hajawahi kukosa kuja kanisani kwa ibada. Wapendwa washarika na vijana wote kwa ujumla,  haijalishi una umaarufu wa kiasi gani usimwache Mungu, fanya kama Msuva Mungu atazidi kukuinua na kubarika kazi ya mikono yako” alisema Mch. Mlyuka.


 Msuva staa wa timu ya Taifa Stars, anayekipiga Wydad Casablanca ya Morroco, ameendelea kuipeperusha na kuitangaza vema bendera ya nchi katika soka kutokana na mafanikio anayoendelea kuyapata huko ughaibuni.


Alianza kuwika na klabu ya Yanga akafanikiwa kuwa staa mkubwa kwenye kikosi chenye wachezaji nyota kwa wakati huo kama Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Amis Tambwe na Haruna Niyonzima na  kufanikiwa kujenga ufalme ndani ya Jangwani.


Kufanya kwake vizuri Yanga kuliwavutia timu ya Difaa Hassani d'el-Jadida ya Morocco na kumnunua kwa zaidi ya milioni 300 huo ulikuwa mwaka 2017.



Baada ya kuwika sana Jadida, Wydad wakavutiwa na kiwango cha Msuva na kuamua kuingia benki na kumnunua kwa Tsh. Bil 1.5 akisaini kandarasi ya miaka minne msimu wa 2020.


Pamoja na juhudi kubwa anazoonyesha kuna kitu ambacho huenda vijana ambao wanacheza soka na wana ndoto za kufika alipo Msuva wanapaswa kufahamu.


Vijana mnaomtazama Msuva kama kioo chenu kuna funzo kubwa hapa, pamoja na juhudi  bidii na kipaji, Tunakumbushwa kumtanguliza Mungu na hata unapopata cheo, au unapokuwa maarufu  usimsahu Mungu kwani atazidi kuibariki kazi yako.