Kocha wa Simba, Pablo Franco, ametetea uamuzi wake wa kucheza bila straika halisi katika mchezo wao wa Jumatano iliyopita dhidi ya Kagera Sugar, mfumo ambao umekuwa ukitumiwa sana na kocha wa Man City ya England, Pep Guardiola.

 


Akizungumza na gazeti la  Championi , kocha Pablo alisema: “Kama kocha, wajibu wangu mkubwa ni kutafuta suluhisho inapotokea tunapitia changamoto fulani. Kabla ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar hatukuweza kufunga bao lolote kwa dakika 180 za michezo miwili mfululizo iliyopita na niliamini tulipaswa kufanya maamuzi ya utofauti.

 

 

“Hapo ndipo tulikuja na wazo la kutumia namba tisa kivuli kwa kujaza viungo wengi na kumtumia Morrison kama straika wetu, kila mmoja ni shuhuda kuwa kwa kiasi fulani tulifanikiwa kutengeneza nafasi lakini kwa bahati mbaya hatukufanikiwa kupata mabao.

 

Katika mchezo huo wa Jumatano iliyopita, Simba hawakuanza na straika yeyote wa asili huku wakianza na viungo sita ambao ni Sadio Kanoute, Rally Bwalya, Clatous Chama, Pape Sakho, Mzamiru Yassin na Bernard Morrison ambaye alicheza kama mshambuliaji.


Chanzo: Championi