Kombe la Mapinduzi linazidi kushika kasi visiwani Zanzibar ambapo msimu huu timu za visiwani zinaonekana kujizatiti na kutoa upinzani mkubwa kwa kwa vigogo kutoka Bara kwa kutandaza soka safi, la mbunu  na la kuvutia.




 

Vigogo hao wa soka bara licha ya kuwa na sehemu kubwa ya vikosi vyao lakini walishindwa kuzibeba pointi tatu kwenye mechi za jana  zikiwa ni za mwisho kwenye makundi yao na waliambulia pointi moja tu.



Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kucheza ambapo walitoshana nguvu na KMKM kwa kufungana mabao 2-2 kisha Simba wao wakashindwa kuziona nyavu za Mlandege na kutoka nao suluhu.


 

Kwa mujibu wa kanuni za Kombe la Mapinduzi zinamtaja kinara wa kundi B ambalo Yanga wamemaliza wakiwazidi KMKM mabao ya kufunga kukutana na kinara wa Kundi A ambapo hadi sasa Azam wakishika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi sita huku wakitarajiwa kumaliza leo Jumamosi dhidi ya Yosso Boys.